Katika blogu hii, tutachunguza njia mbalimbali za kuimarisha ufahamu wetu wa Biblia. Tutajadili mbinu za kusoma Biblia kwa ufanisi, vidokezo vya kukariri maandiko matakatifu, na mikakati ya kutumia somo la Biblia katika maisha yetu ya kila siku. Iwe wewe ni mtaalam wa Biblia mzoefu au unaanza tu safari yako ya imani, "Jifunze Biblia Zaidi" ni rasilimali kamili ya kukusaidia kuongeza ufahamu wako wa Maandiko Matakatifu na kumkaribia Mungu zaidi.

VIJANA NA HATARI INAYOWAKABILI.

 



VIJANA NA HATARI INAYOWAKABILI.

Katika somo hili tutajifunza mambo yafuatayo:-

1.   Wito wa MUNGU kwa vijana

2.   Ni nini kinachoweza kuwafanya vijana wamshinde shetani?

3.   Maovu na makosa katika siku za ujana

Katika siku hizi za mwisho ni vijana wachache sana waliojitoa kikamilifu kumtumikia MUNGU. Wengi wa vijana hata wale walio makanisani wanaishi kwa unafiki, machoni pa watu wakionekana kama watu wa dini, lakini machoni pa MUNGU wakiwa wameoza na kunuka, sababu ya matendo na tabia zao chafu, ingawa si wote. Ningali kijana mdogo niliwahi kuwasikia watu wakidai kuwa dini ni ya wazee. Usemi huu ulimaanisha kuwa,hakuna kijana anaeweza kuwa mcha MUNGU katika siku za ujana,kwamba amewahi kushika dini mno na lazima ataasi tu. Huu ni usemi unaotoka katika kinywa cha shetani mwenyewe. Na kwa ajili hiyo vijana wengi wanaamua kuishi kwa tamaa za mwili wakifanya zinaa wapendavyo na kudhani kuwa wataweza kubadili mielekeo yao pale watakapotaka, maskini watu hawa wamenaswa wavuni mwa shetani na shetani amewamiliki kikamilifu.

Yafuatayo ni baadhi ya matendo mabaya ya vijana wa kizazi hiki.

1.   Utumiaji wa madawa ya kulevya

2.   Tamaa za uasherati

3.   Kuiga na kuvaa nguo na mitindo ya ajabu ya kidunia (vimini,vibode,modo)

4.   Kutowaheshimu wazazi wao.

5.   Kunyoa denge

6.   Kutazama picha chafu

7.   Kula vyakula na vinywaji vya ovyo.

8.   Kupenda miziki na mpira kana kwamba wanashindania uzima wa milele nk.

Vijana wengi wanaishi kana kwamba hakuna MUNGU, na kwa wengi hawamjui MUNGU wala na madai yake kwao. Lakini MUNGU anawaita Vijana;

1.   Wito wa MUNGU kwa Vijana.

“Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako,kabla hazijaja siku zilizo mbaya,wala haijakaribia miaka utakaposema,mimi sina furaha katika hiyo” Mhubiri 12:1.

MUNGU muumbaji anawataka vijana wajitoe kumtumikia; anataka aabudiwe, akumbukwe, ajaliwe, katika siku za ujana, bado una nguvu. Lakini pia fungu hili linataka tuelewe kuwa, baada ya ujana kuna siku zinakuja zilizo mbaya, siku za kukosa furaha.

“Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako , na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote MUNGU atakuleta hukumuni. Kwa hiyo ondoa majonzi moyoni mwako, nawe uondoe ubaya mwilini mwako,kwa maana ujana ni ubatili na utu uzima pia”. Mhubiri 11:9

MUNGU muumbaji anataka kila kijana afurahie ujana wake. Lakini ili ujana upite vizuri-ondoa ubaya mwilini mwako, je ni ubaya gani ulionao? Na utambue ujana ni kama maji ya moto ujana ni ubatili. Na ya kwamba mambo yote ya ujana na utu uzima pia yataletwa hukumuni. Ufanye unalotaka lakini usisahau kuwa katika hayo yote ipo hukumu ya MUNGU inakuja, Jiandae.

 

 

“Vijana rafiki wapendwa, kila mnachopanda mtakivuna pia.sasa ni wakati wenu wa kupanda. Mavuno yatakuwaje? mwapanda nini? Kila neno msemalo, kila tendo mtendalo ni mbegu ambayo itazaa matunda mema au mabaya, nayo italeta furaha au huzuni  kwa mpandaji. Kama ilivyo mbegu iliyopandwa.Ndivyo yatakavyokuwa mavuno. MUNGU amewapa nuru kubwa na mibaraka mingi. Baada ya nuru hiyo kutolewa baada ya hatari kuonyeshwa dhahiri mbele yenu, mambo yanabaki juu yenu. Namna mnavyofaya na nuru ambayo mnapewa na MUNGU italeta furaha ama huzuni. Ninyi wenyewe mnajitayarishaia mwisho wenu wenyewe”. EG White- 1 kutayarisha njia sura ya 35:1 uk.212.

Kila neno msemalo kila tendo mtendalo ni mbegu ambayo itazaa matunda mema au mabaya. Nayo italeta furaha au huzuni kwa mpandaji. Nataka  uelewe kuwa kutowaza sahihi tu kwa dakika moja, kutenda jambo dogo tu ambalo si la haki, kunaweza kubadiri mkondo wa maisha yako yote; Ninyi wenyewe mnajitayarishia mwisho wenu.

“Muda mfupi unaotumika katika kupiga maisha ujanani, rafiki zangu vijana wapendwa, utatoa mazao ambayo yatafanya maisha yako yote yawe machungu, saa moja ya kutowaza sahihi, mara unapokubali kuingia katika jaribu, waweza kubadilisha mkondo mzima wa maisha kwenda mwelekeo usio sahihi. Unao ujana mmoja tu, hebu ufanye kuwa wenye manufaa. Upitapo katika eneo moja huwezi kurejea na kurekebisha makosa yako. Shetani huwa anajigeuza na kuwa mfano wa malaika wa nuru ajapo kwa vijana na majaribu yake yanayohadaa na huwa anafanikiwa kuwashinda, hatua kwa hatua kutoka katika wajibu wao”. EG.White – 1 Maranatha uk 82:1-2.

Ni kweli shetani ajapo kwa vijana na majaribu yake tena yanayohadaa anafanikiwa kuwashinda. Ni wengi ambao shetani amewashinda kwa tamaa za mwili, kwa ulevi wa pombe, ulafi, na kwa kutowatii wazazi wao. Vijana hawa ambao ndio hufanya familia, taifa na kisha mataifa, wengi wao wamearibika kiasi kikubwa. Katika Mataifa mbalimbali hata vijana wanavyoongea tu ushuhudia jambo hili na wengine wanaongea kama mazezeta, wenyewe wakijiita kuwa ni masela; huu wote ni upotevu wa maadili.

MUNGU anahitaji maisha ya ujana juu ya vijana tulio nao katika nyumba zetu na kanisani, maisha yao yawe kielelezo:     - Kielelezo katika usemi

-      Kielelezo katika mwenendo

-      Kielelezo katika upendo

-      Kielelezo katika imani

-      Kielelezo katika mavazi, uvae kwa kujistiri. Maandiko yanaendelea  kuonya ifuatavyo:-

“Mtu awaye yote asiudharau ujana wako,bali uwe kielelezo kwao waaminio,katika usemi na mwenendo na katika upendo na imani na usafi”. 1 Timotheo 4:12.

Ili ujana wako usidharauliwe uwe kielelezo katika mwenendo, usemi, upendo, kielelezo katika imani, utakuwa na ujana wenye manufaa. Lakini kama mwenendo wako ni wa ovyo, usemi ni waovyo, watu hawataacha kukudharau. Je wewe kijana unaesoma kitabu hiki ulichonacho mkononi mwako, mwenendo wako ukoje? Je, watu wanavyo kutazama wanaona kielelezo katika imani na usafi? Habari gani juu ya usemi wako, Maana katika siku hizi za mwisho kuna lugha zinazotumika mitaani ambazo zinaonyesha upotovu wa maadili. Zifuatazo ni baadhi ya lugha zinazotumiwa na vijana lakini ni upotofu wa maadili cha ajabu hata vijana Wakristo nao wamepotoka.

(i)          Shilingi elfu moja- inaitwa buku, sijui hii nitafasiri ya lugha gani duniani.

(ii)        Shilingi mia tano – inatwa jero.

 

(iii)       Baba – anaitwa dingi, lakini ukweli dingi ni mdudu ambae husukuma mavi kinyume nyume, Maajabu kabisa.

(iv)       Masela, demu, nisepe, sharobaro, mshikaji, ganja nk.

Lakini vijana Wakristo siyo kwamba wanapaswa kuepuka kutumia lugha hizi tu, bali wao watabaki kuwa vielelezo katika usemi safi.Lakini kumbukumbu zinaonyeshaje? Hata vijana wakristo wengi wao wamepotoka. MUNGU kupitia nabii wake akuacha kuonya;

“Katika mazungumzo ya siku hizi kuna lugha zisizofaa zenye kutia hofu (masela, demu, dingi, jero, nisepe, mshikaji). Lugha hizi zinaonyesha hali duni ya mawazo na hali duni ya maadili.Heshima ya kweli katika tabia ni nadra sana.Wapo watu wachache tu ambao ni safi na wasiotiwa unajisi. Hatari za kimaadili ambazo zinawakabili wote wazee kwa vijana, zinaongezeka kila siku.Kuharibika kwa maadili,ambako tunakuita upotovu unapata nafasi ya kutosha kutenda kazi na wanaume, wanawake, na vijana ambao wanadai kuwa Wakristo, wataacha mvuto ambao ni duni, wa kupenda anasa, na wa kishetani”. EG. White - 1 Maranatha 153: 1,4.

·         Hizi ni lugha zisizofaa

·         Zinaonyesha upotovu wa maadili

·         Zinaonyesha hali duni ya mawazo ya wanaume na wanawake.

·         Wote wale wanaozitumia wanaacha mvuto wa kishetani.

·         Wote wale wanaozitumia ni wapenda anasa

·         Wamebaki watu wachache ambao ni safi katika usemi na ambao hawajatiwa unajisi.

Neno linaendelea kuonya.

“Wala aibu wala maneno ya upuuzi wala ubishi hayo hayapendezi, bali afadhali kushukuru. Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyokuwa na maana kwa sababu ya hayo hasira ya MUNGU huwajia wana wa uasi  Waefeso 5:4,6.

“Neno lolote lililo ovu lisitoke kinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuitaji ili liwape neema wanaosikia Waefeso 4:29.

Maneno maovu:

(i)          Lugha zisizofaa (upotevu wa maadili)

(ii)        Maneno ya upuuzi

(iii)       Maneno yasiyo na maana

(iv)       Maneno ya aibu.

(v)         Maneno ya ubishi

(vi)       Maneno ya utani (hata na mashemeji na binamu).

Maneno maovu mengine; masela, demu, dingi, buku, nisepe, jero, mshikaji, sharobaro, lugha hizi zinaonyesha hali duni ya mawazo na hali duni ya maadili. Na wanaume kwa wanawake na vijana wanaojidai kuwa wakristo lakini wanazungumza maneno maovu kama haya; neno linasema, wanaacha mvuto wa kishetani.Hata hivyo neno linaendelea kuonya ifuatavyo:-

“Basi nawaambia, kila nemo lisilo na maana watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki na kwa maneno yako utahukumiwa”.  Mathayo 12:36-37.

 

 

 

2.   Nini kinachoweza kuwafanya vijana wamshinde shetani.

Je, vijana wanauwezo wa kumshinda shetani? Ndiyo. Yafuatayo ni makundi mbalimbali ya watu waliomo kanisani wenye uwezo wa kumshinda shetani, wakiwemo na vijana.

“Nawaandikia ninyi akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi vijana kwa sababu mmemshinda yule mwovu.Nimewaandikia ninyi watoto kwa sababu mmemjua

baba.Nimewandikia ninyi vijana kwa sababu mna nguvu na neno la MUNGU inakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu”. 1 Yohana 2:13-14.

Kuna watu wengi sana wanaogelea katika maovu siku za ujana wao.Wanatenda maovu mpaka yanakera katika siku za ujana, wakidhani wataweza kubadili mambo watakavyotaka, na wengine kwa unyoge wanadhani hawawezi kumshinda Ibilisi katika siku za ujana, huo ni uongo. Neno la MUNGU linathibitisha kuwa vijana wanao uwezo wa kumshinda shetani. Lakini ili wapate kumshinda shetani ni mpaka neno la MUNGU likae kwa wingi ndani yao. Hii ndiyo siri ya kushinda dhambi katika siku za ujana.

“Kutokana na yale niliyoonyeshwa, si zaidi ya nusu ya vijana wanaodai kuamini dini na kweli ambao wameongoka kwelikweli. Majina yameandikwa katika vitabu vya Kanisa hapa duniani, lakini sio katika kitabu cha uzima. Naliona kuwa katika vijana hakuna hata mmoja kati ya ishirini anayejua hasa maisha ya dini yalivyo hasa”. EG. White - 1T 504; MYP 384 [1867] Dhiki kuu uk 51:2-3

Narudia tena; ni nini kinachomfanya mtu asitende dhambi?

“Moyoni mwangu nimeliweka neno lako nisije (mimi) nikakutenda dhambi”. Zaburi 119:11.

Kwa kutojua haya vijana wengi wanaishi kwa unafiki, machoni pa watu wakionekana kama watu wema. Lakini machoni pa MUNGU wakiwa wameoza na hata kunuka.Kama kuna kijana ananuka kwa vitendo viovu, ifuatayo ndio njia ya kujisafisha; liko tumaini la kunukia tena. “Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii akilifuata neno la MUNGU”. Zaburi 119:9.

“Usiogope maana hutatahayarika wala usifadhaike maana hutaaibishwa kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako” Isaya 54:4.

Kama unanuka kwa tabia na matendo mabaya, kanisani, nyumbani, mtaani, pengine umekuwa mvuta bangi, mwizi, usiyeheshimu hata wazazi wako, mara ngapi umetembea nusu uchi mabarabarani, pengine umewai hata kujiuza na kufanya viungo vya mwili wako kuwa kiwanda cha kuchapisha hela; umetumia madawa ya kulevya, nguo zenyewe hata sasa unavaa modo, Kata kei, nguo zingine unavaa zimetobolewa matundu, unatembea viungo vya mwili wako viko nje, haujisitiri tena kama Biblia inavyofundisha. Kwa haya yote na mengine mengi ingawa waweza kujipaka marashi ukitembea unanukia; lakini ukweli katika haki unanuka. Machoni pa watu waliopotoka pia waweza kuonekana maridadi na hata wakakusifu, lakini machoni pa MUNGU mkuu, unakaribia hukumu yako, sababu ya vitendo vyako viovu.

Pamoja na hayo liko tumaini kwa vijana wale watakaoona imetosha waishie hapo kunuka kwa tabia mbaya; Namna ya kujisafisha ni kwa kutii na kulifuata neno la MUNGU, utakuwa umepata ushindi mkuu dhidi ya Ibilisi. Na MUNGU wetu atakusafisha hata uweze kunukia kwa tabia njema na wala siyo kwa malashi. Umebarikiwa sana kuijua siri ya ushindi wa dhambi katika siku za ujana.

 

“Hebu vijana wafundishwe kujifunza kwa makini neno la MUNGU. Likipokelewa rohoni litakuwa kizuizi kikubwa dhidi ya majaribu. Mtunga Zaburi anasema; “Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, nisije nikakutenda dhambi; kwa neno la midomo yako nimejiepusha na njia za wenye jeuri” (Zaburi 119:11, 17:4).Kama mashauri ya neno la MUNGU yakifuatwa kwa uaminifu, neema ya Kristo inayookoa italetwa kwa vijana wetu; Kwani watoto wanaofundishwa kupenda na kumtii MUNGU na wanaojitoa wenyewe kwa

uwezo wake wenye nguvu wa neno lake linalounda ndiyo shabaha ya uangalizi maalumu na Baraka za MUNGU”. EG.White - 2 katika Ulimwengu wa Roho Uk 34:4-5.

Umebarikiwa sana kuijua siri ya ushindi wa dhambi katika siku za ujana. Hebu sasa nakusii umgeukie MUNGU na neno lake, utakuwa umebadili kabisa maisha yako toka mwelekeo usio sahihi, kwenda mwelekeo ulio sahihi, na ukijiandaa kuishi maisha ya milele katika mji wa MUNGU. Neno linaendelea kuwaita vijana:-

“Ni vema mwanadamu aichukue nira wakati wa ujana wake” Maombolezo 3:27.

Je, Nira ambayo vijana wanapaswa kuichukua wakati wa ujana ni nini?

“Nira hiyo ni sheria za MUNGU ,ambazo zimeandikwa ndani ya mioyo.Humuunganisha mtenda kazi wa MUNGU na mapenzi ya MUNGU.Kama tungaliachwa kuenenda jinsi tupendavyo,tungelitumbukia katika mashimo ya shetani.Kwa hiyo MUNGU hutufunga katika mapenzi yake”. EG.White - Tumaini la Vizazi Vyote Sura 34.Uk.180.

Mojawapo ya neno, ama maandiko ambayo kijana anapaswa kuyashika ni sheria ya MUNGU. Ifuatayo ndiyo nira ama sheria ya MUNGU ambayo itiiwe siku za ujana.

Kutoka 20:1-17

1.   Usiwe na Miungu mingine ila mimi

2.   Usijifanyie sanamu ya kuchonga

3.   Usilitaje bure jina la BWANA MUNGU wako.

4.   Ikumbuke siku ya sabato uitakase

5.   Waheshimu baba yako na mama yako

6.   Usiue

7.   Usizini

8.   Usiibe

9.   Usimshuhudie jirani yako uongo.

10.     Usitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako.

Nimeiandika kwa ufupi hebu soma Kutoka 20:1-17.

Amri kumi ndiyo Nira ambayo kila kijana anapaswa kuichukua na kwa njia hiyo atakuwa amefungwa katika mapenzi ya MUNGU na kujihepusha na maisha machungu ya baadaye.Neno la MUNGU likipokelewa rohoni katika siku za ujana litakuwa kizuizi kikubwa dhidi ya majaribu, na litakuvika ustiri mtakatifu.

“Mioyo ya vijana ikiachwa bila kuzuiwa inaelekezwa kwenye mkondo unaopatana na tabia yao iliyoharibika, wanaacha kuwa macho na kujihadhari na kupeana upendo kila mmoja na mwenzake, kuwa na marafiki maalumu watu maalumu wa kuwatunzia siri na wakati marafiki hawa wanapokuwa pamoja,Yesu hatajwi sana kati yao.mazungumzo yao hayahusu maisha ya Kikristo, hayamhusu Kristo, hayahusu mbinguni bali yako katika mambo ya upuuzi.Hawafahamu hila za mwovu na wakiwa

 

kwenye umri wa miaka kumi na mbili,kumi na nne,kumi na tano, na kumi na sita,wanajifikiria kuwa ni vijana wakubwa wa kike na wakiume na kwamba wanauwezo wa kuchagua mwelekeo wao wenyewe na kujiongoza wenyewe kwa adabu na uangalifu”. EG. White – 2 Katika Ulimwengu wa Roho 38:4-5.

3.   Makosa na Maovu katika siku za ujana.

Wale wote wanaojiona wana uwezo wa kujiongoza wenyewe kwa sababu wamesoma elimu ya ulimwengu, ama kwa kuwa wana uchumi, au kwa vile, wanatoka katika ukoo ulio bora, wataishia katika maovu makuu. Neno la MUNGU ndio kizuizi kikubwa dhidi ya dhambi,si kwa vijana tu bali na kwa watu wote duniani. Hebu ufanye ujana wako kuwa wenye manufaa kwa kutii neno, utakuwa unaishi kwa viwango vya mbinguni na siyo kwa viwango vya ulimwengu.

Lakini kwa kutoyajua haya, kwa wengi miaka ya ujana ni siku za kupiga maisha. Wengine kwa kutazama picha chafu kwenye mitandao, tamaa za uasherati, kucheza mziki, kula na kunywa vyakula vya ovyo na vya kianasa, kunyoa denge, kuvaa nguo za mitindo ya ajabu ya kidunia (modo, kata keyi, vimini, vibode) utumiaji wa madawa ya kulevya, kujikoboa, kutowaheshimu wazazi wao, na hata wizi; haya ni baadhi tu ya maovu yanayotendeka katika siku za ujana.

“Tunaishi katika kipindi cha upotovu na Wanaume kwa vijana ni jasiri katika dhambi. Vijana wetu wasipolindwa kwa utakatifu, wasipolindwa kwa kanuni thabiti, uangalizi mkubwa usipodhihirishwa katika kuchagua rafiki zao pamoja na machapisho yanayolisha akili, watakuwa wameachiliwa kwa jamii ambayo maadili yao yamechafuka kama yalivyokuwa ya wakazi wa Sodoma. Vijana wetu watakutana na majaribu kila upande na ni lazima waelimishwe kwamba itawapasa wategemee nguvu itokayo juu, kuliko yale yatolewayo na binadamu”. EG. White – 2 Wana na Binti za Mungu uk 47:1.

Ni kwambie ndugu msomaji; ni vigumu kuyaandika maasi yote ya ujana katika somo hili. Kwani makosa na dhambi nyingi watu wengi hutenda wakati wa ujana, na hii ni kwa sababu wamemkataa MUNGU. Mtumishi wa MUNGU Daudi alipojua haya akasema ifuatavyo:

“Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu, wala maasi yangu, unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako, Ee BWANA kwa ajili ya wema wako” Zaburi 25:7.

Ndugu msomaji kama si wema wa MUNGU, na kama si fadhili za MUNGU tu, kama akiyakumbuka maovu na maasi ya ujana wako nani angesimama? Hata na mimi kwa kuyaandika haya ni kwa wema wa MUNGU tu sistahili. Hebu ombi la Daudi na liwe ombi letu, tumlilie MUNGU afute dhambi zetu na asiyakumbuke maovu na maasi ya ujana wetu. Ingawa vijana wengi wanajipaka marashi nakutembea wananukia lakini kwa ajili ya maovu na maasi yao machoni pa haki wananuka, je, wewe unayesoma haya kwa tabia yako unadhani unanukia ama unanuka, tafakari. Yafuatayo ni baadhi tu ya makosa mengine ya ujana ambayo vijana wa kiume na wa kike wanapaswa kuyashinda.

(i)                  Tamaa.

“Lakini uzikimbie tamaa za ujanani, ukafuate haki, na imani, na upendo na amani, pamoja na wale wamwitao BWANA kwa moyo safi” 2 Timotheo 2:22.

Nataka uelewe kuwa kwenye ujana kuna tamaa. Na vijana mnapaswa kuzikimbia tamaa za ujanani. Na hili uzikimbie ni mpaka uwe mwenye imani, upendo safi, mwenye haki, na ufuatane pamoja na wale wamwitao BWANA kwa moyo safi. Kuna watu wengi hata

 

makanisani wanamtaja BWANA kwa kuimba, Kwa kuhubiri, lakini si kwa moyo safi. Uwe macho, usije ukarudia tabia za kishenzi wakati uko kanisani.

“Wengine wanahubiri habari za kristo kwa sababu ya husuda na fitina ,wengine kwa nia njema. Hawa wana mhubiri kwa pendo,wakijua ya kuwa nimewekwa ili niitetee injili,bali wengine wanamhubiri kristo kwa fitina,wala si kwa moyo mweupe”. Wafilipi 1:15-17. Soma pia Mathayo 7:21,

Lakini uzikimbie tamaa za ujanani; ni tamaa gani? “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia, na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele”. 1Yohana 2:15 -17.

Tamaa ambazo vijana wanapaswa kuzikimbia.

(i)   Tamaa ya mwili

(ii)  Tamaa ya macho

(iii) Na kiburi cha uzima

Wote watakao yang’anga’nia haya wataangamia na tamaa zao. Ishi kwa kutenda mapenzi ya MUNGU na utadumu milele ukiwa katika mji wa MUNGU.

“Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi Tito 2:6.

 Maonyo:

“Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipinganazo na roho” 1 Petro 2:11.

Na mabinti nao; “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu kwa paa na kwa ayala wa porini, msiyachochee mapenzi, wala kuyaamusha, hata yatakapoona vema yenyewe” Wimbo bora 3:5

(i)          Kuacha wazi sehemu nyeti za mwili, mfano, kitovu, mapaja, matiti tumbo, ni kutangaza kuyaamsha mapenzi

(ii)        Kuvaa nguo fupi za kubana, zinaamsha mapenzi

(iii)       Kujipamba kwa kujikoboa. Vijana wote wa kiume na wa kike, na kama mapenzi unaona yanajichochea mwilini kwa tamaa ujizuie. Na kama unashindwa kujizuia ni aibu. “Bali yeye asiyejizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai” 1Timotheo 5:6 kuishi kwa tamaa ni uovu mkuu. Hata hivyo mpango mwingine wa kupinga tamaa huu hapa chini:-

“Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane ni heri wakae kama mimi nilivyo. Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe, maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa”. 1Wakoritho 7:8-9.

Vijana wengine hukwepa kuoa wakidai Maisha ni magumu na huku wakiendelea kufanya uzinzi, ingawa hakuna siku maisha yatakuwa rahisi. Wanabadilisha wanawake kama nguo wakidhani wanawakomesha kumbe wanajikomesha wenyewe. Wasichana wengine nao wanaona maisha ya ndoa ni ya utumwa na hawata kuwa na uhuru, na hivyo wanaonelea afadhali waishi wakibadilisha wanaume kama nguo, ilimradi anapata riziki

 

ya kuishi. Kwa ajili hiyo kitendo cha ndoa kilichotolewa na kubarikiwa kiwe furaha kwao waliooana leo kimegeuzwa kuwa mradi wa kutafutia fedha. Maajabu kabisa.

Ifuatayo ni dawa ya kutiisha tamaa za mwili.

“MUNGU anataka vijana kuwa watu wenye mioyo hodari, kutayarishwa kuitenda kazi yake bora,na kufanya wafae kuchukua madaraka. MUNGU anawaita vijana wenye mioyo safi wenye nguvu na hodari, na wenye kukusudia kupigana kiume katika vita vilivyo mbele yao, ili wapate kumtukuza MUNGU, na kuwanufaisha wanadamu. Ikiwa vijana wangeifanya Biblia kuwa somo lao, wangeweza kutuliza tamaa zao mbaya, na kusikiliza sauti ya muumbaji wao. Licha ya kuwa na amani na MUNGU, hata wangejiona kuwa wameadilishwa na kuzidishwa hadhi” EG. White -1 Kutayalisha njia Sura ya... uk 214:2.

Ufuatao ndio mpango wa MUNGU juu ya miili yetu;

”Maana haya ndiyo mapenzi ya MUNGU, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati, kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima,si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua MUNGU. Maana MUNGU hakutuitia uchafu, bali tuwe katika utakaso”. 1 Watesalonike 4:3-5,7.

Je, mwili wako unakushinda kujizuia kwa tamaa? Basi wewe ni maiti unaetembea, maana andiko lasema” Bali yeye asiyejizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai” 1Timotheo 5:6.

Wale waliotakaswa na neno la MUNGU wazingatie yafuatayo:-

·                     Kila mmoja wetu ajue kuuweza mwili wake

·                     Mwili uwe katika hali ya heshima

·                     Mwili uwe katika hali ya utakatifu

·                     Mwili usiwe katika hali ya uchafu, Maana MUNGU hakutuitia uchafu

·                     Na mwili usiwe katika hali ya tamaa mbaya, kama watu wa mataifa wasiomju MUNGU, yaani wapagani. Kufaamu kwa kina zaidi juu ya jambo hili hebu nikuombe fanya kila unaloweza kupata kitabu kile cha amri kumi na usome amri ya saba inayosema usizini. Utabarikiwa sana na utakuwa umeongeza kina cha ujuzi wa kumjua MUNGU.

 

(ii)                Makosa ya ujana, lingine ni kutoheshimu wazazi

“Msikilize baba yako aliyekuzaa wala usimdharau mama yako akiwa mzee”. Mithali 23:22.

Wazazi wengi wanaombembeleza, wana huzuni, na wengine wanauchungu kwa sababu ya tabia na matendo ya vijana wao maana yanakera,unaweza kuishia kushangaa kumuona kijana wa miaka kumi na tano,  au hata miaka ishirini, anavuta sigara, bangi, anavaa nguo, lakini nguo ya ndani ndiyo iko nje, hata katika suruali zao ni kama ndani yake amebeba mzigo wa mavi. Matendo kama haya na mengine kwa mzazi makini yatamtia uchungu.

“Mwana mpumbavu ni huzuni kwa babaye, na uchungu kwa mamaye aliyemzaa”. Mithali 17:25.

   “Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye bali mwana mpumbavu ni mzigo wa mamaye”. Mithali 10:1.

 

Ni kweli wapo watoto ambao wanawapa matunzo na heshima nzuri baba na mama zao,na hawa bila shaka hufurahisha wazazi wao. Lakini katika familia nyingi wapo watoto ambao ni mzigo. Wameharibu miili na akili zao sababu ya uvutaji wa bangi na sigara. Kila siku hawakosi vijiweni na kwenye makundi ya watu wahuni. Si hivyo tu wengine wamekuwa mzigo sababu hata kufanya kazi kwa mikono yao hawataki, ni wavivu. “Ikiwa mtu hataki kufanya kazi basi asile chakula”. 2 Watesalonike 3:10-11.

Watoto hawa ambao ndio hufanya taifa kisha mataifa wameharibika kiasi kikubwa, hivyo karibu ulimwengu wote umeharibika kimaadili, ingawa bado kuna watu wachache wenye Roho wa MUNGU. Watoto wa kike nao kuna wengine wanalaani kuolewa,wakidhani kuolewa ni utumwa. Wengi wao wamebadilisha viungo vyao vya uzazi na kuwa viwanda vya kutengeneza hela, na mwisho wao, wameambulia magonjwa mazito, na wengine kuzaa ovyo ovyo na hatimaye kuwa mzigo nyumbani mwao. Laiti ungekubali maonyo ya wazazi wako ungejiokoa na maovu.

Na alaaniwe amdharauye baba yake na mama yake na watu wote waseme amina”. Kumbukumbu la Torati 27:16 kufahamu vizuri jinsi ya kuwaheshimu wazazi, hebu tafuta kitabu kile cha amri kumi za MUNGU na usome amri ya tano, utabarikiwa sana.

TAMAA YA MACHO: Kutamani vitu vya watu kumewafanya vijana wengine kugeuka kuwa wezi. Wizi au kuiba ni kitendo cha kutamani mali ya mtu mwingine na hatimaye kuamua kuchukua, kuficha, kulagahai, au kunyang’anya, na kujitwalia bila ridhaa ya mwenyewe. Dhambi hii ya wizi ni tatizo kubwa katika jamii linatokana na tabia iliyojengwa zaidi katika msingi wa tamaa na ubinafsi. Na vijana wengi katika familia mbalimbali kwa sababu ya kutokupenda kufanya kazi na uvivu hugeuka kuwa wanyang’anyi ama wadokoaji.

“Maana adhulumuye atapata mapato ya udhalimu wake wala hakuna upendeleo” Wakolosai 3:25.

“Msiwe na tabia ya kupenda fedha, mwe radhi na vitu mlivyonavyo kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha”. Waebrania 13:5.

“Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yoyote niliyo nayo. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa, katika hali yoyote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”. Wafilipi 4:11-13.

“Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hali hiyo wamefarakana na imani na kujichoma kwa maumivu mengi”. 1 Timotheo 6:10.

(iii)               Kosa lingine katika siku za ujana, ni kutazama picha chafu.

Shetani ambaye hapendi maadili mema ameingiza uharibifu katika baadhi ya vyombo vya habari. Vitabu vya hadithi za mapenzi, video, magazeti, TV, Internate, Simu nk. Vitu hivi vimebeba uchafu unaochafua mawazo ya vijana wengi. Asilimia kubwa ya yale yaliyomo katika vitu hivi ni shule inayoelekeza wengi kwenda kwenye umalaya. Mengi yaliyopitia machoni na kusikia kwa masikio yamekuwa chanzo cha watu wengi kuharibika. Wale wanaopenda maisha yao watachaghua vile vya kuona, kusoma na kusikiliza. Kuingia katika shule ya umalaya kwa kuangalia na kusoma visivyofaa kutaharibu afya yako, akili yako. Na mwisho ni kuangamia milele. MUNGU muumbaji kupitia kwa Nabii wake.  E.G.White, anaandika ifuatavyo juu ya jambo hili;

 

“Hata hivyo bado tunayokazi ya kufanya ili kupinga majaribu. Wale ambao hawataanguka katika mbinu za shetani wanapaswa kulinda vizuri maeneo ya nafsi; wanapaswa kujizuia kusoma, kuona, au

kusikia kile kitakacholeta mawazo machafu. Akili haipaswi kuachwa itangetange huku na huko katika kila kitakachopendekezwa na adui wa roho. E.G.White - 1W/Manabii 465:3 pp 460:2

Hata hivyo mtumishi wa MUNGU Daudi akiwa katika njozi takatifu MUNGU alimwambia aandike ifuatavyo; “Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, unihuishe katika njia yako” Zaburi 119:37

 

Watu wengi katika simu zao wanapicha za wanawake walio uchi, na Wasichana wengine nao hupiga picha za ajabu kabisa na kuzituma kwenye mtandao wao wenyewe, ili wanaume wawaone walivyoumbika. Hata saluni nyingi zimepambwa ukutani na picha za hivyo, hakika hiki ni kizazi kilichopotoka sana, kizazi cha zinaa. Unaweza kushangaa kuona baba mzima tena na kitambi chake anaangalia picha za ngono, hili ni janga. Wasomi wengi nao ni wahanga wa janga hili, unaweza kuishia kushangaa kuwaona watu wanaodaiwa kuwa wameelimika kwa kupata elimu ya ulimwengu, na kumbe ndio wamepotoka kabisa, ingawa sio wote. Nikwambie ndugu msomaji elimu kuu kuliko elimu zote ni ya Biblia. Kama haujapata elimu ya Biblia, basi bado una ulemavu katika mambo ya elimu. Kutazama dhambi, yaani, kutazama picha za ngono kwenye mitandao na kusoma hadithi za mapenzi - ni uzinzi; ni uvunjaji wa amri ya saba. Hebu sasa nikuombe usome hapa chini kwa makini sana;

 

“Vijana wengi wana shauku ya vitabu. Wanasoma kila kitu wanachoweza kukipata. Hadithi za kusisimua za mapenzi na picha chafu zina mvuto wenye kupotosha. Vitabu vya hadithi za kubuni vinasomwa na wengi, na matokeo yake ni kwamba fikra za  wengi zinanajisika. Ndani ya magari, picha za wanawake ambao wako uchi zinasambazwa kwa ajili ya kuuzwa. Picha hizi zenye kuchukiza zinaninginizwa kwenye kuta za wale wanaofanya biashara ya kutia nakshi. Hiki ni kizazi ambacho upotovu unaenea kila mahali. Tamaa ya macho na ya mwili inaamushwa kwa kutazama na kusoma. Moyo unachafuliwa kwa njia ya fikra. Akili inapendezwa kufikiria matukio yanayoamusha tamaa mbaya. Picha hizi zenye kutia aibu, ambazo zinatazamwa kupitia fikra zilizonajisiwa, zinaharibu tabia na kumwandaa mtu ambaye amedanganyika na kupumbazwa na upendo, ashindwe kujizuia katika tamaa za mwili. Ndipo inafuata dhambi na uhalifu ambavyo vinawavuta wanadamu ambao wameumbwa kwa mfano wa MUNGU, kwenda chini kabisa hadi kufikia kiwango sawa na mnyama, na katimaye kuwazamisha katika uangamivu. Epuka  kusoma na kuangalia mambo ambayo yataleta mawazo mabaya. Hebu akili zetu zisidhoofishwe na kupotoshwa hata kwa kusoma vitabu vya hadithi.”  E.G.White - 1 Maranatha 143:1

Hatima ya Vijana na watu wote watakaodumu kutenda maovu;

“Mimi nalisema nawe wakati wa kufanikiwa kwako, lakini ulisema, sitaki kusikia. Hii ndiyo iliyokuwa desturi yako tangu ujana wako, kutokutii sauti yangu”Yeremia 22:21.

“Na tulale kwa aibu yetu, haya yetu na itufunike; kwa maana tumemwasi BWANA, MUNGU wetu, sisi na baba zetu tangu ujana wetu hata leo. Wala hatukutii sauti ya BWANA, MUNGU wetu”. Yeremia 3:25.

Wito

“Hakika baada ya kugeuzwa kwangu nalitubu; na baada ya kufundishwa kwangu, nalijipiga pajani; nalitahayarika, naam, nalifadhaika, kwa sababu naliichukua aibu ya ujana wanguYeremiah 31:19.

“Maana ujapojiosha kwa magadi, na kujipatia sabuni nyingi, lakini uovu wako umeandikwa mbele zangu, asema BWANA MUNGU”. Yeremia 2:22.

 

Fanya maamuzi sasa ya kuishi kwa mpango wa MUNGU, ukitii neno lake na amri kumi zake, na utakuwa umepata ushindi mkuu dhidi ya Ibilisi katika siku za ujana. Kumbuka,

ukimgeukia MUNGU katika siku za ujana, utakuwa umejiandaa vyema kubeba majukumu ya kazi ya MUNGU. Ukiwa na utambuzi na maarifa, tofauti na mtu aliyearibu ujana kwa kupiga maisha.

 

“Historia ya Mfalme wa kwanza wa Israeli inaonyesha mfano wenye huzuni wa nguvu za awali katika mazoea. Wakati wa ujana wake Sauli hakumpenda wala kumcha Mungu; na Roho ya kutokuwa na subira, akiwa hakufundishwa mapema kujitoa, alikuwa tayari kuasi mamlaka ya Mbinguni. Wale ambao wakati wa ujana wao hujali mambo matakatifu kwa ajili ya mapenzi ya Mungu, na ambao wanatekeleza Wajibu katika nafasi zao kwa uaminifu, wataandaliwa kushika majukumu makubwa baadaye. Lakini wanadamu hawawezi kwa miaka mingi kupotosha nguvu ambazo Mungu amewapa, na kisha, wanapochagua kubadilika, wanazikuta nguvu hizi zikiwa mpya na huru kwa ajili ya kuzifanyia kazi iliyo kinyume na iliyokusudiwa”. EG. White – PP 622;2, 2 Wazee na Manabii uk 686:2.

BWANA akubariki na karibu katika Kanisa la Mungu.

Share:

Maoni 1 :

  1. How to win at a slot machine in Vegas | DrmCD
    It 과천 출장안마 is 양주 출장마사지 not a 충청북도 출장마사지 fun game to play because 전라남도 출장샵 many people can't seem to realize this before it. 양산 출장샵 The goal is to get more and more at a slot machine

    JibuFuta

Popular Posts

Lebo

Recent Posts

Pages